Eze. 7:9-16 Swahili Union Version (SUV)

9. Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, napiga.

10. Angalia, siku hiyo; angalia, inakuja; ajali yako imetokea; fimbo imechanua, kiburi kimechipuka.

11. Udhalimu umeinuka, ukawa fimbo ya uovu; hapana mtu atakayesalia miongoni mwao, wala katika jamii yao, wala kitu katika utajiri wao; wala hakutakuwa kutukuka kati yao.

12. Majira yamewadia, siku ile inakaribia; huyo anunuaye asifurahi, wala asihuzunike auzaye; maana ghadhabu imewapata wote jamii.

13. Kwa maana auzaye hatakirudia kilichouzwa, wajapokuwa wangali hai; kwa sababu maono haya yawahusu wote jamii; hapana mmoja atakayerudi; wala hapana mtu atakayejitia nguvu katika uovu wa maisha yake.

14. Wamepiga tarumbeta, wameweka vitu vyote tayari; lakini hapana aendaye vitani; maana ghadhabu yangu imewapata wote jamii.

15. Upanga uko nje, na tauni na njaa zimo ndani; yeye aliye nje mashambani atakufa kwa upanga; na yeye aliye ndani ya mji, njaa na tauni zitamla.

16. Lakini watakaokimbia watakimbia, nao watakuwa juu ya milima kama hua wa bondeni, wote wakilia, kila mmoja katika uovu wake.

Eze. 7