1. Nawe, mwanadamu, ujipatie upanga mkali, kama wembe wa kinyozi ujipatie, ukaupitishe juu ya kichwa chako na ndevu zako; kisha ujipatie mizani ya kupimia, ukazigawanye nywele hizo.
2. Theluthi ya hizo utaiteketeza katikati ya mji, siku za mazingiwa zitakapotimia; nawe utatwaa theluthi, na kuipiga kwa upanga pande zote; nawe utatawanya theluthi ichukuliwe na upepo, nami nitafuta upanga nyuma yake.
3. Nawe twaa nywele chache katika hizo, na kuzifunga katika upindo wa mavazi yako.
4. Nawe utatwaa tena baadhi ya hizo, na kuzitupa katikati ya moto, na kuziteketeza katika moto huo; kutoka nywele hizo moto utakuja na kuingia katika nyumba yote ya Israeli.
5. Bwana MUNGU asema hivi; Huu ndio Yerusalemu; nimeuweka kati ya mataifa, na nchi zauzunguka pande zote.
6. Nao umeasi hukumu zangu, kwa kutenda mabaya kuliko mataifa hayo, nao umeasi sheria kuliko nchi hizo ziuzungukazo; maana wamezikataa hukumu zangu, wala hawakuenda katika sheria zangu.
7. Basi, kwa hiyo Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu ninyi mmefanya ghasia kuliko mataifa wawazungukao ninyi, wala hamkuenda katika sheria zangu, wala hamkuzishika hukumu zangu, wala hamkutenda kama kawaida za mataifa wawazungukao;
8. basi, Bwana MUNGU asema hivi; Angalia, mimi, naam, mimi, ni juu yako; nami nitafanya hukumu kati yako machoni pa mataifa.
9. Nami nitakutenda nisiyoyatenda zamani, wala sitafanya tena mambo kama hayo, kwa sababu ya machukizo yako yote.
10. Kwa sababu hiyo baba za watu watawala wana wao kati yako, nao wana watawala baba zao; nami nitafanya hukumu ndani yako, na hao wote waliosalia kwako nitawatawanya kwa pepo zote.
11. Kwa sababu hiyo, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hakika kwa kuwa umepatia unajisi patakatifu pangu, kwa matendo yako yote niyachukiayo, na kwa machukizo yako yote, kwa sababu hiyo mimi nami nitakupunguza; wala jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma.
12. Theluthi yenu mtakufa kwa tauni, na kwa njaa watakomeshwa ndani yako; na theluthi yenu wataanguka kwa upanga pande zako zote; na theluthi yenu nitawatawanya kwa pepo zote, kisha nitafuta upanga nyuma yao.