1. Basi, haya ndiyo majina ya kabila hizo; toka mwisho wa pande za kaskazini, karibu na njia ya Hethloni, hata maingilio ya Hamathi, hata Hasar-enoni, penye mpaka wa Dameski, yaani, upande wa kaskazini karibu na Hamathi, watakuwa na upande wa mashariki, na upande wa magharibi; Dani fungu moja.
2. Tena mpakani mwake Dani, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Asheri, fungu moja.
3. Na mpakani mwa Asheri, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Naftali, fungu moja.
4. Na mpakani mwa Naftali, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Manase, fungu moja.
5. Na mpakani mwa Manase, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Efraimu, fungu moja.
6. Na mpakani mwa Efraimu, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Reubeni, fungu moja.
7. Na mpakani mwa Reubeni, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; Yuda, fungu moja.
8. Na mpakani mwa Yuda, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi, yatakuwapo matoleo mtakayotoa, upana wake mianzi ishirini na tano elfu, na urefu wake sawasawa na moja la mafungu hayo, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; na mahali patakatifu ni katikati yake.
9. Matoleo hayo, mtakayomtolea BWANA, urefu wake ni mianzi ishirini na tano elfu, na upana wake elfu kumi.
10. Matoleo hayo matakatifu yatakuwa kwa watu hawa, kwa makuhani; upande wa kaskazini urefu wake ishirini na tano elfu, na upande wa magharibi upana wake elfu kumi, na upande wa mashariki upana wake elfu kumi, na upande wa kusini urefu wake ishirini na tano elfu; na mahali patakatifu pa BWANA patakuwa katikati yake.
11. Patakuwa kwa makuhani wa wana wa Sadoki, waliotakasika, walioulinda ulinzi wangu, wasioasi, wana wa Israeli walipoasi, kama Walawi walivyoasi.
12. Na matoleo hayo ya nchi yatolewayo, yatakuwa kwao kitu kitakatifu sana, karibu na mpaka wa Walawi.