Eze. 46:3-13 Swahili Union Version (SUV)

3. Watu wa nchi nao wataabudu mbele ya mlango wa lile lango mbele za BWANA, siku za sabato, na siku za mwezi mpya.

4. Nayo sadaka ya kuteketezwa, ambayo mkuu atamtolea BWANA siku ya sabato, itakuwa wana-kondoo sita wakamilifu, na kondoo mume mkamilifu.

5. Na sadaka ya unga itakuwa efa moja kwa kondoo mume, na sadaka ya unga kwa wale wana-kondoo, kiasi awezacho kutoa, na hini moja ya mafuta kwa efa moja.

6. Na siku ya mwezi mpya itakuwa ni ng’ombe mume mchanga mkamilifu; na wana-kondoo sita, na kondoo mume; nao watakuwa wakamilifu.

7. Naye atatengeneza sadaka ya unga, efa moja kwa ng’ombe mume, na efa moja kwa kondoo mume, na kwa wale wana-kondoo, kwa kiasi awezacho kutoa, na hini moja ya mafuta kwa efa moja.

8. Naye mkuu atakapoingia, ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango lile, naye atatoka kwa njia iyo hiyo.

9. Lakini watu wa nchi watakapokuja mbele za BWANA katika sikukuu zilizoamriwa, yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kaskazini ili kuabudu, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kusini; na yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kusini, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kaskazini; hatarudi kwa njia ya lango aliloingia kwalo, lakini atatoka kwa kwenda mbele moja kwa moja.

10. Naye mkuu atakapoingia, ataingia katikati yao, nao, watakapotoka, watatoka wote pamoja.

11. Na katika sikukuu hizo, na sikukuu nyingine zilizoamriwa, sadaka ya unga itakuwa efa moja kwa ng’ombe mmoja, na efa moja kwa kondoo mume mmoja, na kwa wale wana-kondoo kiasi awezacho kutoa, na hini moja ya mafuta kwa efa moja.

12. Naye mkuu atakapotengeneza sadaka atoayo kwa hiari yake mwenyewe, sadaka ya kuteketezwa, au sadaka za amani, ziwe sadaka amtoleazo BWANA kwa hiari yake mwenyewe, mtu mmoja atamfungulia lango lile lielekealo upande wa mashariki, naye ataitengeneza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka zake za amani, kama afanyavyo siku ya sabato; kisha atatoka; na baada ya kutoka kwake mtu mmoja atalifunga lango.

13. Nawe utatengeneza mwana-kondoo wa mwaka wa kwanza, mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA kila siku; kila siku asubuhi utamtengeneza.

Eze. 46