Eze. 44:7-19 Swahili Union Version (SUV)

7. kuwa mmewaingiza wageni, ambao mioyo yao haikutahiriwa, wala miili yao haikutahiriwa, wawe ndani ya patakatifu pangu, wapatie unajisi, naam, nyumba yangu, mtoapo sadaka ya chakula changu, mafuta na damu; nao wameyavunja maagano yangu, juu ya machukizo yenu yote.

8. Wala hamkuvilinda vitu vyangu vitakatifu bali mmejiwekea walinzi wa kawaida zangu, katika patakatifu pangu.

9. Bwana MUNGU asema hivi; Hapana mgeni, ambaye moyo wake haukutahiriwa, wala mwili wake haukutahiriwa, atakayeingia patakatifu pangu, miongoni mwa wageni walio kati ya wana wa Israeli.

10. Lakini Walawi waliofarakana nami, hapo Waisraeli walipopotea, waliopotea na kuvifuata vinyago vyao, watachukua uovu wao wenyewe.

11. Hata hivyo watakuwa wahudumu katika patakatifu pangu, wakiwa wasimamizi wa malango ya nyumba, wakihudumu humo nyumbani; watawachinjia watu sadaka za kuteketezwa na dhabihu, nao watasimama mbele yao ili kuwahudumia.

12. Kwa sababu waliwahudumia mbele ya vinyago vyao, wakawa kwazo la uovu kwa nyumba ya Israeli; basi nimeuinua mkono wangu juu yao, asema Bwana MUNGU, nao watachukua uovu wao.

13. Wala hawatanikaribia, kunihudumia katika kazi ya ukuhani, wala hawatakaribia vitu vyangu vitakatifu kimojawapo, vitu vilivyo vitakatifu sana; bali watachukua aibu yao, na machukizo yao yote waliyoyatenda.

14. Lakini nitawafanya kuwa walinzi katika ulinzi wa nyumba, kwa huduma yake yote, na kwa yote yatakayotendeka ndani yake.

15. Lakini makuhani Walawi, wana wa Sadoki, waliolinda ulinzi wa patakatifu pangu, hapo wana wa Israeli walipopotea na kuniacha, hao ndio watakaonikaribia ili kunihudumia; nao watasimama mbele zangu, kunitolea mafuta na damu, asema Bwana MUNGU;

16. wataingia patakatifu pangu, nao wataikaribia meza yangu, ili kunihudumia, nao watalinda ulinzi wangu.

17. Itakuwa, hapo watakapoingia kwa malango ya ua wa ndani, watavikwa mavazi ya kitani; wala sufu haitakuwa juu yao, maadamu wanahudumu katika malango ya ua wa ndani, na ndani ya nyumba.

18. Watakuwa na vilemba vya kitani juu ya vichwa vyao, nao watakuwa na suruali za kitani viunoni mwao; hawatajifunga kiunoni kitu cho chote kifanyacho jasho.

19. Nao watakapotoka kuingia ua wa nje, yaani, ua wa nje wa watu, ndipo watakapoyavua mavazi yao waliyovaa katika huduma yao, na kuyaweka katika vile vyumba vitakatifu, nao watavaa mavazi mengine, wasije wakawatakasa watu kwa mavazi yao.

Eze. 44