Eze. 44:4-14 Swahili Union Version (SUV)

4. Kisha akanileta, kwa njia ya lango la upande wa kaskazini, mbele ya nyumba; nikaangalia, na tazama, huo utukufu wa BWANA uliijaza nyumba ya BWANA; nikaanguka kifudifudi.

5. BWANA akaniambia, Mwanadamu, weka moyoni mwako, ukatazame kwa macho yako, ukasikie kwa masikio yako, maneno yote nitakayokuambia, katika habari ya kawaida zote za nyumba ya BWANA, na ya amri zake zote; nawe weka moyoni mwako maingilio ya nyumba, pamoja na matokeo yote ya mahali patakatifu.

6. Nawe utawaambia waasi, yaani nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Enyi nyumba ya Israeli, katika machukizo yenu yote, na iwatoshe,

7. kuwa mmewaingiza wageni, ambao mioyo yao haikutahiriwa, wala miili yao haikutahiriwa, wawe ndani ya patakatifu pangu, wapatie unajisi, naam, nyumba yangu, mtoapo sadaka ya chakula changu, mafuta na damu; nao wameyavunja maagano yangu, juu ya machukizo yenu yote.

8. Wala hamkuvilinda vitu vyangu vitakatifu bali mmejiwekea walinzi wa kawaida zangu, katika patakatifu pangu.

9. Bwana MUNGU asema hivi; Hapana mgeni, ambaye moyo wake haukutahiriwa, wala mwili wake haukutahiriwa, atakayeingia patakatifu pangu, miongoni mwa wageni walio kati ya wana wa Israeli.

10. Lakini Walawi waliofarakana nami, hapo Waisraeli walipopotea, waliopotea na kuvifuata vinyago vyao, watachukua uovu wao wenyewe.

11. Hata hivyo watakuwa wahudumu katika patakatifu pangu, wakiwa wasimamizi wa malango ya nyumba, wakihudumu humo nyumbani; watawachinjia watu sadaka za kuteketezwa na dhabihu, nao watasimama mbele yao ili kuwahudumia.

12. Kwa sababu waliwahudumia mbele ya vinyago vyao, wakawa kwazo la uovu kwa nyumba ya Israeli; basi nimeuinua mkono wangu juu yao, asema Bwana MUNGU, nao watachukua uovu wao.

13. Wala hawatanikaribia, kunihudumia katika kazi ya ukuhani, wala hawatakaribia vitu vyangu vitakatifu kimojawapo, vitu vilivyo vitakatifu sana; bali watachukua aibu yao, na machukizo yao yote waliyoyatenda.

14. Lakini nitawafanya kuwa walinzi katika ulinzi wa nyumba, kwa huduma yake yote, na kwa yote yatakayotendeka ndani yake.

Eze. 44