6. Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kuume, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arobaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia.
7. Nawe utauelekeza uso wako, uelekee mazingiwa ya Yerusalemu, na mkono wako utakuwa haukuvikwa nguo, nawe utatoa unabii juu yake.
8. Na tazama, nitakutia pingu, wala hutageuka toka upande mmoja hata upande wa pili, hata utakapozitimiza siku za mazingiwa yako.
9. Pia ujipatie ngano, na shayiri, na kunde, na dengu, na mtama, na kusemethi, ukavitie vyote katika chombo kimoja, ukajifanyie mkate kwa vitu hivyo; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala ubavuni mwako; yaani, siku mia tatu na tisini utaula.
10. Na chakula chako utakachokula kitapimwa, shekeli ishirini kwa siku moja; utakila kwa wakati wake.
11. Nawe utakunywa maji kwa kuyapima, sehemu ya sita ya hini; utayanywa kwa wakati wake.
12. Nawe utakila kama mkate wa shayiri, nawe utakioka mbele ya macho yao juu ya mashonde yatokayo katika mwanadamu.
13. BWANA akasema, Hivyo ndivyo wana wa Israeli watakavyokula chakula chao, hali kimetiwa unajisi, kati ya mataifa nitakakowafukuza.