4. Tena lala chini kwa ubavu wako wa kushoto, ukaweke huo uovu wa nyumba ya Israeli juu yake; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala juu yake, kwa kadiri hiyo utauchukua uovu wao.
5. Maana nimekuagizia miaka ya uovu wao iwe kwako hesabu ya siku, yaani, siku mia tatu na tisini; ndivyo utakavyouchukua uovu wa nyumba ya Israeli.
6. Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kuume, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arobaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia.
7. Nawe utauelekeza uso wako, uelekee mazingiwa ya Yerusalemu, na mkono wako utakuwa haukuvikwa nguo, nawe utatoa unabii juu yake.
8. Na tazama, nitakutia pingu, wala hutageuka toka upande mmoja hata upande wa pili, hata utakapozitimiza siku za mazingiwa yako.
9. Pia ujipatie ngano, na shayiri, na kunde, na dengu, na mtama, na kusemethi, ukavitie vyote katika chombo kimoja, ukajifanyie mkate kwa vitu hivyo; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala ubavuni mwako; yaani, siku mia tatu na tisini utaula.
10. Na chakula chako utakachokula kitapimwa, shekeli ishirini kwa siku moja; utakila kwa wakati wake.