6. Nami nitapeleka moto juu ya Magogu; na juu ya watu wote wakaao salama katika visiwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
7. Na jina langu takatifu nitalifanya kuwa limejulika kati ya watu wangu Israeli; wala sitaliacha jina langu takatifu kutiwa unajisi tena; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, na Aliye Mtakatifu katika Israeli.
8. Tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU; hii ndiyo siku ile niliyoinena.
9. Hao wakaao katika miji ya Israeli watatoka, nao watafanya mioto kwa silaha za vita na kuziteketeza, ngao, na vigao, na pinde, na mishale, na mafumo, na mikuki, nao watazitumia kama kuni kwa muda wa miaka saba;
10. hata hawataokota kuni mashambani, wala hawatakata kuni msituni; maana watafanya mioto kwa silaha zile; nao watawateka nyara watu waliowateka wao, na kunyang’anya vitu vya watu walionyang’anya vitu vyao, asema Bwana MUNGU.
11. Tena, itakuwa katika siku hiyo, nitampa Gogu pa kuzikia katika Israeli, bonde la wapitao, upande wa mashariki wa bahari; nalo litawazuia wapitao; na huko watamzika Gogu na watu wake jamii yote; nao wataliita, Bonde la Hamon-Gogu.
12. Na kwa muda wa miezi saba nyumba ya Israeli watakuwa wakiwazika, wapate kuisafisha nchi.
13. Naam, watu wote wa nchi hiyo watawazika; itakuwa ni sifa kwao katika siku ile nitakapotukuzwa, asema Bwana MUNGU.
14. Nao watawachagua watu wa kufanya kazi ya daima, watakaopita kati ya nchi, ili kuwazika waliosalia juu ya uso wa nchi, ili kuisafisha; miezi saba itakapokwisha kupita watatafuta.
15. Na hao wapitao kati ya nchi watatafuta; na mtu ye yote aonapo mfupa wa mtu, ndipo atakapoweka alama karibu nao, hata wazishi watakapouzika katika bonde la Hamon-Gogu.