7. basi Bwana MUNGU asema hivi; Nimeinua mkono wangu, kusema, Hakika, mataifa walio karibu nanyi pande zote, wao watachukua aibu yao.
8. Lakini ninyi, enyi milima ya Israeli, mtachipuza matawi yenu na kuwapa watu wangu Israeli matunda yenu; maana wa karibu kuja.
9. Maana, tazama, mimi nasimama upande wenu, nami nitawaelekea, nanyi mtalimwa na kupandwa mbegu;
10. nami nitaongeza watu juu yenu, nyumba yote ya Israeli, naam, yote pia; nayo miji itakaliwa na watu, na mahali palipoharibika patajengwa.
11. Nami nitaongeza juu yenu mwanadamu na mnyama, nao watazidi na kuzaa; nami nitawakalisha watu ndani yenu, kwa kadiri ya hali yenu ya kwanza, nami nitawatendea mema kuliko mema ya mianzo yenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
12. Naam, nitaleta watu watembee juu yenu, naam, watu wangu Israeli; nao watakumiliki, nawe utakuwa urithi wao, wala hutawafisha watoto wao tena tangu leo.
13. Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa watu hukuambia, wewe nchi u mwenye kula watu, nawe umekuwa mwenye kufisha watu wa taifa lako;