1. Na wewe, mwanadamu, itabirie milima ya Israeli, useme, Enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la BWANA.
2. Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu adui amesema juu yenu, Aha! Na, Mahali pa juu pa zamani pamekuwa petu tupamiliki;
3. basi tabiri useme, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu, naam, kwa sababu wamewafanya ninyi kuwa ukiwa, na kuwameza pande zote, mpate kuwa milki kwa mabaki ya mataifa, nanyi mmeambwa kwa midomo yao waongeao, na kwa masingizio ya watu;
4. kwa sababu hiyo, enyi milima ya Israeli, lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU aiambia hivi hiyo milima na vilima, mifereji ya maji na mabonde, mahali palipoharibika na kuwa ukiwa, na miji iliyoachwa na watu, ambayo imekuwa mateka, na kuzomewa na mabaki ya mataifa, walio karibu pande zote;