Eze. 34:8-15 Swahili Union Version (SUV)

8. Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo zangu walikuwa mateka, kondoo zangu wakawa chakula cha wanyama-mwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo zangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo zangu;

9. kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA;

10. Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao.

11. Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia.

12. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza.

13. Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu.

14. Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli.

15. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU.

Eze. 34