Eze. 34:20-31 Swahili Union Version (SUV)

20. Kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU awaambia hivi; Tazama, mimi, naam, mimi, nitahukumu kati ya wanyama walionona na wanyama waliokonda.

21. Kwa kuwa mmesukuma kwa ubavu, na kwa mabega, na kuwapiga wenye maradhi kwa pembe zenu, hata mkawatawanyia mbali;

22. basi mimi nitaliokoa kundi langu, wala hawatakuwa mateka tena; nami nitahukumu kati ya mnyama na mnyama.

23. Nami nitaweka mchungaji mmoja juu yao, naye atawalisha, naam, mtumishi wangu, Daudi; yeye atawalisha, naye atakuwa mchungaji wao.

24. Na mimi, BWANA, nitakuwa Mungu wao, na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mkuu kati yao; mimi, BWANA, nimesema haya.

25. Nami nitafanya agano la amani nao, nami nitawakomesha wanyama wakali kati yao; nao watakaa salama jangwani, na kulala misituni.

26. Nami nitawafanya wao, na mahali palipo pande zote za mlima wangu, kuwa baraka, nami nitaleta manyunyu kwa wakati wake; yatakuwako manyunyu ya baraka.

27. Na mti wa kondeni utazaa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, nao watakuwa salama katika nchi yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapovunja vifungo vya kongwa lao, na kuwaokoa katika mikono ya watu wale waliowatumikisha.

28. Hawatakuwa mateka ya makafiri tena, wala mnyama wa nchi hatawala; bali watakaa salama salimini, wala hapana mtu atakayewatia hofu.

29. Nami nitawainulia miche iwe sifa njema, wala hawataangamizwa kwa njaa katika nchi yao tena, wala hawatachukua tena aibu ya makafiri.

30. Nao watajua ya kuwa mimi, BWANA, Mungu wao, ni pamoja nao, na ya kuwa wao, nyumba ya Israeli, ni watu wangu, asema Bwana MUNGU.

31. Na ninyi, kondoo zangu, kondoo za malisho yangu, ni wanadamu, na mimi ni Mungu wenu, asema Bwana MUNGU.

Eze. 34