Eze. 34:13-25 Swahili Union Version (SUV)

13. Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu.

14. Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli.

15. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU.

16. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.

17. Na kwa habari zenu, Enyi kundi langu, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nahukumu kati ya mnyama na mnyama, kondoo waume na mbuzi waume pia.

18. Je! Mwaona ya kuwa ni neno dogo ninyi kulishwa malisho mema, hata mkawa hamna budi hukanyaga kwa miguu yenu yaliyosalia? Na kuwa mmekunywa maji yaliyo safi, nanyi hamna budi kuyatibua kwa miguu yaliyobaki?

19. Na kwa habari za kondoo zangu, wao wanakula hayo mliyoyakanyaga kwa miguu yenu, nao wanakunywa maji mliyoyatibua kwa miguu yenu.

20. Kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU awaambia hivi; Tazama, mimi, naam, mimi, nitahukumu kati ya wanyama walionona na wanyama waliokonda.

21. Kwa kuwa mmesukuma kwa ubavu, na kwa mabega, na kuwapiga wenye maradhi kwa pembe zenu, hata mkawatawanyia mbali;

22. basi mimi nitaliokoa kundi langu, wala hawatakuwa mateka tena; nami nitahukumu kati ya mnyama na mnyama.

23. Nami nitaweka mchungaji mmoja juu yao, naye atawalisha, naam, mtumishi wangu, Daudi; yeye atawalisha, naye atakuwa mchungaji wao.

24. Na mimi, BWANA, nitakuwa Mungu wao, na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mkuu kati yao; mimi, BWANA, nimesema haya.

25. Nami nitafanya agano la amani nao, nami nitawakomesha wanyama wakali kati yao; nao watakaa salama jangwani, na kulala misituni.

Eze. 34