14. Ndipo nitakapoyafanya maji yao kuwa safi, na kuiendesha mito yao kama mafuta, asema Bwana MUNGU.
15. Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa na jangwa, nchi iliyopungukiwa na vitu vilivyoijaza, nitakapowapiga watu wote wakaao ndani yake, ndipo watakapojua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
16. Hayo ndiyo maombolezo watakayoomboleza; binti za mataifa wataomboleza kwa hayo; kwa hayo wataomboleza kwa ajili ya Misri, na kwa ajili ya watu wake wote jamii, asema Bwana MUNGU.
17. Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, siku ya kumi na tano ya mwezi, neno la BWANA likanijia kusema,
18. Mwanadamu, walilie watu wa Misri. Wote jamii ukawabwage, naam, yeye, na binti za mataifa mashuhuri, hata pande za chini za nchi, pamoja na watu washukao shimoni.
19. Umemshinda nani kwa uzuri? Shuka, ukalazwe pamoja na wasiotahiriwa.
20. Wataanguka kati ya watu waliouawa kwa upanga; ametokwa apigwe na upanga; mvuteni aende mbali pamoja na watu wake wote jamii.
21. Walio hodari watasema naye, toka kati ya kuzimu pamoja nao wamsaidiao; wameshuka wamelala kimya, hata wasiotahiriwa, hali wameuawa kwa upanga.
22. Ashuru yuko huko, na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga,
23. ambao makaburi yao yamewekwa pande za shimo zilizo mbali sana, wote jamii wamezunguka kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, waliofanya utisho katika nchi yao walio hai.
24. Elamu yuko huko, na watu wake wote jamii, pande zote za kaburi lake; wote pia wameuawa, wameanguka kwa upanga, walioshuka hali hawana tohara hata pande za chini ya nchi; ambao waliwatia watu hofu katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni.
25. Wamemwekea kitanda kati ya hao waliouawa, pamoja na watu wake wote jamii; makaburi yake yamzunguka; wote pia hawakutahiriwa, wameuawa kwa upanga; maana maogofyo yao yalifanyika katika nchi ya walio hai, nao wamechukua aibu yao, pamoja nao washukao shimoni; amewekwa kati ya hao waliouawa.