1. Ikawa katika mwaka wa kumi na mbili, mwezi wa kumi na mbili, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema,
2. Mwanadamu, mfanyie Farao, mfalme wa Misri, maombolezo, umwambie, Ulifananishwa na mwana-simba wa mataifa; lakini umekuwa kama joka katika bahari; nawe watoka kwa nguvu pamoja na mito yako, na kuyachafua maji kwa miguu yako, na kuitia uchafu mito yao.
3. Bwana MUNGU asema hivi; Nitautanda wavu wangu juu yako, kwa kusanyiko la watu wa kabila nyingi; nao watakuvua katika jarife langu.
4. Nami nitakuacha juu ya nchi kavu, nitakutupa juu ya uso wa uwanda, nami nitawaleta ndege wote wa angani watue juu yako, nami nitawashibisha wanyama wa dunia yote kwako wewe.
5. Nami nitaweka nyama yako juu ya milima, na kuyajaza mabonde kwa urefu wako.
6. Tena kwa damu yako nitainywesha nchi, ambayo waogelea juu yake, hata milimani; na mifereji ya maji itajawa nawe.
7. Nami nitakapokuzimisha, nitazifunikiza mbingu, na kuzifanya nyota zake kuwa giza; nami nitalifunika jua kwa wingu, wala mwezi hautatoa nuru yake.
8. Mianga yote ya mbinguni iangazayo nitaifanya kuwa giza juu yako, nami nitatia giza katika nchi yako, asema Bwana MUNGU.