5. Kushi, na Putu, na Ludi, na watu wote waliochanganyika, na Kubu, na wana wa nchi ya agano, wataanguka kwa upanga pamoja nao.
6. BWANA asema hivi; Nao pia wanaoitegemeza Misri wataanguka, na kiburi cha uwezo wake kitashuka; toka Migdoli hata Sewene, wataanguka ndani yake kwa upanga, asema Bwana MUNGU.
7. Nao watakuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake itakuwamo kati ya miji iliyoharibika.
8. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoweka moto katika Misri, na hao wote wamsaidiao watakapoangamia.
9. Katika siku hiyo watatoka wajumbe mbele zangu katika merikebu, ili kuwatia hofu Wakushi, wanaojiona kuwa salama, na dhiki itakuwa juu yao, vile vile kama katika siku ya Misri; kwa maana, tazama, inakuja.
10. Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaukomesha wingi wa watu wa Misri, kwa mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli.
11. Yeye, na watu wake pamoja naye, watu wa mataifa watishao, wataletwa waingie katika nchi waiharibu, nao watafuta panga zao wapigane na Misri, na kuijaza nchi wale waliouawa.
12. Nami nitaikausha mito, na kuiuza nchi, na kuitia katika mikono ya watu wabaya; nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa, na watu wote walio ndani yake, kwa mkono wa wageni; mimi, BWANA, nimenena neno hili.
13. Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaviharibu vinyago, nami nitavikomesha vitu vya ubatili katika Nofu, wala hapatakuwa na mkuu tena atokaye katika nchi ya Misri, nami nitatia hofu katika nchi ya Misri.
14. Nami nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa, nami nitatia moto katika Soani, nami nitatekeleza hukumu katika No.
15. Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Sini, ngome ya Misri, nami nitakatilia mbali wingi wa watu wa No.
16. Nami nitatia moto katika Misri; Sini itakuwa katika dhiki kuu, na No itavunjika kabisa; na Nofu itakuwa na adui wakati wa mchana.
17. Vijana wa Oni, na wa Pi-besethi, wataanguka kwa upanga; na miji hiyo itakwenda utumwani.
18. Huko Tapanesi nako mchana utakuwa giza, nitakapovunja huko kongwa za Misri, na kiburi cha uwezo wake kitakoma ndani yake, na katika habari zake, wingu litaifunika, na binti zake watakwenda utumwani.
19. Hivyo ndivyo nitakavyotekeleza hukumu katika Misri; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
20. Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa kwanza, siku ya saba ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema,
21. Mwanadamu, nimeuvunja mkono wa Farao, mfalme wa Misri, na tazama, haukufungwa ili kuutia dawa, haukuzongwa kwa kitambaa, upate kuwa na nguvu za kushika upanga.
22. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya Farao, mfalme wa Misri, nami nitamvunja mikono yake, mkono ulio wenye nguvu, na huo uliovunjika, nami nitauangusha upanga ulio katika mkono wake.