1. Neno la BWANA likanijia tena, kusema,
2. Mwanadamu, tabiri, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Pigeni makelele ya uchungu, Ole wa siku ile!
3. Kwa maana siku ile i karibu, siku ile ya BWANA i karibu, siku ya mawingu; itakuwa wakati wa mataifa.
4. Na upanga utakuja juu ya Misri, na dhiki itakuwa katika Kushi, watakapoanguka watu waliouawa katika Misri, nao watauondoa wingi wa watu wake, na misingi yake itabomolewa.
5. Kushi, na Putu, na Ludi, na watu wote waliochanganyika, na Kubu, na wana wa nchi ya agano, wataanguka kwa upanga pamoja nao.
6. BWANA asema hivi; Nao pia wanaoitegemeza Misri wataanguka, na kiburi cha uwezo wake kitashuka; toka Migdoli hata Sewene, wataanguka ndani yake kwa upanga, asema Bwana MUNGU.
7. Nao watakuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake itakuwamo kati ya miji iliyoharibika.
8. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoweka moto katika Misri, na hao wote wamsaidiao watakapoangamia.