4. Nami nitatia kulabu katika taya zako, nami nitawashikamanisha samaki wa mito yako na magamba yako; nami nitakutoa katika mito yako, pamoja na samaki wa mito yako walioshikamana na magamba yako.
5. Nami nitakuacha hali umetupwa jangwani, wewe na samaki wote wa mito yako; utaanguka juu ya uso wa uwanda; hutakusanywa, wala kuwekwa pamoja; nimekutoa uwe chakula cha wanyama wa nchi, na cha ndege wa angani.
6. Na watu wote wakaao Misri watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, kwa sababu wamekuwa mwanzi wa kutegemewa kwa nyumba ya Israeli.
7. Walipokushika kwa mkono wako, ulivunjika, ukawararua mabega yao yote; nao walipokutegemea, ulivunjika, ukawatetemesha viuno vyao vyote.
8. Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitaleta upanga juu yako, nami nitakatilia mbali nawe wanadamu na wanyama.
9. Nayo nchi ya Misri itakuwa ukiwa na jangwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; kwa sababu amesema, Mto huu ni wangu, nami nimeufanya.
10. Basi, tazama, mimi ni juu yako, na juu ya mito yako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa tupu, na ukiwa, toka Migdoli hata Sewene, hata mpaka wa Kushi.
11. Hautapita kati yake mguu wa mwanadamu, wala hautapita kati yake mguu wa mnyama, wala haitakaliwa na watu, muda wa miaka arobaini.
12. Nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake, kati ya miji iliyoharibika, itakuwa maganjo muda wa miaka arobaini; nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, nami nitawatapanya kati ya nchi mbalimbali.
13. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Mwisho wa miaka arobaini nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hizo kabila za watu, ambazo walitawanyika kati yao;
14. nami nitawarejeza Wamisri walio katika hali ya kufungwa, nami nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni.