1. Neno la BWANA likanijia tena, kusema,
2. Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu.
3. Tazama, una hekima kuliko Danieli; hapana neno la siri watu wawezalo kukuficha;
4. kwa hekima yako na kwa fahamu zako umejipatia utajiri, nawe umepata dhahabu na fedha katika hazina zako;
5. kwa hekima yako nyingi, na kwa biashara yako, umeongeza utajiri wako, na moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako;
6. basi, kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu;
7. basi, tazama, nitaleta wageni juu yako, watu wa mataifa wenye kutisha; nao watafuta panga zao juu ya uzuri wa hekima yako, nao watautia uchafu mwangaza wako.
8. Watakushusha hata shimoni; nawe utakufa kifo chao waliouawa kati ya bahari.
9. Je! Utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, Mimi ni Mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha.
10. Utakufa kifo cha hao wasiotahiriwa, kwa mikono ya wageni; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.
11. Tena neno la BWANA likanijia, kusema,
12. Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri.
13. Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.