24. Hao ndio waliokuwa wachuuzi wako, kwa vitu vya tunu, kwa vitumba vya nguo za samawi na kazi ya taraza, na masanduku ya mavazi ya thamani, yaliyofungwa kwa kamba, na kufanyizwa kwa mti wa mierezi, katika bidhaa yako.
25. Merikebu za Tarshishi zilikuwa misafara yako, kwa bidhaa yako; nawe ulijazwa sana, ukawa mtukufu sana, katika moyo wa bahari.
26. Wavuta makasia wako walikuleta katika maji makuu; upepo wa mashariki umekuvunja moyoni mwa bahari.
27. Mali zako, na bidhaa yako, na utajiri wako, wana-maji wako, na rubani zako, na wenye kutia kalafati wako, na wafanya biashara wako, na watu wako wa vita wote, walio ndani yako, pamoja na jeshi lako lote lililo ndani yako, wataanguka katika moyo wa bahari katika siku ya kuangamia kwako.
28. Kwa sauti ya vilio vya rubani zako viunga vyako vitatetema.
29. Na wote wavutao kasia, wana-maji, na rubani zote wa baharini, watashuka katika merikebu zao, na kusimama katika nchi kavu;
30. nao watasikizisha watu sauti zao juu yako, nao watalia kwa uchungu, na kutupa mavumbi juu ya vichwa vyao, na kugaagaa katika majivu;
31. nao watajifanya kuwa na upaa kwa ajili yako, na kujifunga nguo za magunia viunoni, nao watakulilia kwa uchungu wa roho, kwa maombolezo ya uchungu.
32. Na katika kulia kwao watakufanyia maombolezo, na kukuombolezea, wakisema, Ni nani aliye kama Tiro, kama yeye aliyenyamazishwa kati ya bahari?
33. Bidhaa zako zilipotoka katika bahari, uliwajaza watu wa kabila nyingi; uliwatajirisha wafalme wa dunia, kwa wingi wa mali zako, na kwa utajiri wako.
34. Wakati ulipovunjwa na bahari, katika vilindi vya maji, bidhaa zako na jeshi lako lote walianguka kati yako.
35. Wote wakaao katika visiwa vile watakustaajabia, na wafalme wao wameogopa sana, wamefadhaika nyuso zao.
36. Wafanya biashara kati ya kabila za watu wakuzomea; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena milele.