17. Yuda, na nchi ya Israeli, walikuwa wachuuzi wako; walitoa badala ya bidhaa yako ngano ya Minithi, na mtama, na asali, na mafuta, na zeri.
18. Dameski alikuwa mfanya biashara kwako, kwa habari ya wingi wa kazi za mkono wako, kwa ajili ya wingi wa aina zote za utajiri; akaleta divai ya Helboni, na sufu nyeupe.
19. Wedani, na Yavani, walifanya biashara toka Uzali kwa vitu vyako; chuma kilichofuliwa, na mdalasini, na mchai, vilikuwa katika bidhaa yako.
20. Dedani alikuwa mchuuzi wako, kwa nguo za thamani za kutandikia farasi.
21. Arabuni, na wakuu wote wa Kedari, ndio waliokuwa wafanya biashara wa mkono wako; kwa wana-kondoo, na kondoo waume, na mbuzi; kwa hao walifanya biashara nawe.
22. Wachuuzi wa Sheba, na Raama, ndio waliokuwa wachuuzi wako; badala ya vitu vyako walitoa manukato yaliyo mazuri, na kila aina ya vito vya thamani, na dhahabu.
23. Harani, na Kane, na Adini, wachuuzi wa Sheba, na Ashuru, na Kilmadi, walikuwa wachuuzi wako.
24. Hao ndio waliokuwa wachuuzi wako, kwa vitu vya tunu, kwa vitumba vya nguo za samawi na kazi ya taraza, na masanduku ya mavazi ya thamani, yaliyofungwa kwa kamba, na kufanyizwa kwa mti wa mierezi, katika bidhaa yako.
25. Merikebu za Tarshishi zilikuwa misafara yako, kwa bidhaa yako; nawe ulijazwa sana, ukawa mtukufu sana, katika moyo wa bahari.
26. Wavuta makasia wako walikuleta katika maji makuu; upepo wa mashariki umekuvunja moyoni mwa bahari.
27. Mali zako, na bidhaa yako, na utajiri wako, wana-maji wako, na rubani zako, na wenye kutia kalafati wako, na wafanya biashara wako, na watu wako wa vita wote, walio ndani yako, pamoja na jeshi lako lote lililo ndani yako, wataanguka katika moyo wa bahari katika siku ya kuangamia kwako.
28. Kwa sauti ya vilio vya rubani zako viunga vyako vitatetema.
29. Na wote wavutao kasia, wana-maji, na rubani zote wa baharini, watashuka katika merikebu zao, na kusimama katika nchi kavu;
30. nao watasikizisha watu sauti zao juu yako, nao watalia kwa uchungu, na kutupa mavumbi juu ya vichwa vyao, na kugaagaa katika majivu;