14. Watu wa nyumba ya Togarma walifanya biashara, kwa farasi, naam, farasi za vita, na nyumbu, wapate vitu vyako vilivyouzwa.
15. Wadedani walikuwa wachuuzi wako, visiwa vingi vilikuwa soko la mkono wako; walikuletea pembe, na mpingo, ili kuvibadili.
16. Shamu alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa kazi za mkono wako walifanya biashara kwa zumaridi, na urujuani, na kazi ya taraza, na kitani safi, na marijani, na akiki, wapate vitu vyako vilivyouzwa.
17. Yuda, na nchi ya Israeli, walikuwa wachuuzi wako; walitoa badala ya bidhaa yako ngano ya Minithi, na mtama, na asali, na mafuta, na zeri.
18. Dameski alikuwa mfanya biashara kwako, kwa habari ya wingi wa kazi za mkono wako, kwa ajili ya wingi wa aina zote za utajiri; akaleta divai ya Helboni, na sufu nyeupe.
19. Wedani, na Yavani, walifanya biashara toka Uzali kwa vitu vyako; chuma kilichofuliwa, na mdalasini, na mchai, vilikuwa katika bidhaa yako.
20. Dedani alikuwa mchuuzi wako, kwa nguo za thamani za kutandikia farasi.
21. Arabuni, na wakuu wote wa Kedari, ndio waliokuwa wafanya biashara wa mkono wako; kwa wana-kondoo, na kondoo waume, na mbuzi; kwa hao walifanya biashara nawe.
22. Wachuuzi wa Sheba, na Raama, ndio waliokuwa wachuuzi wako; badala ya vitu vyako walitoa manukato yaliyo mazuri, na kila aina ya vito vya thamani, na dhahabu.
23. Harani, na Kane, na Adini, wachuuzi wa Sheba, na Ashuru, na Kilmadi, walikuwa wachuuzi wako.
24. Hao ndio waliokuwa wachuuzi wako, kwa vitu vya tunu, kwa vitumba vya nguo za samawi na kazi ya taraza, na masanduku ya mavazi ya thamani, yaliyofungwa kwa kamba, na kufanyizwa kwa mti wa mierezi, katika bidhaa yako.
25. Merikebu za Tarshishi zilikuwa misafara yako, kwa bidhaa yako; nawe ulijazwa sana, ukawa mtukufu sana, katika moyo wa bahari.
26. Wavuta makasia wako walikuleta katika maji makuu; upepo wa mashariki umekuvunja moyoni mwa bahari.
27. Mali zako, na bidhaa yako, na utajiri wako, wana-maji wako, na rubani zako, na wenye kutia kalafati wako, na wafanya biashara wako, na watu wako wa vita wote, walio ndani yako, pamoja na jeshi lako lote lililo ndani yako, wataanguka katika moyo wa bahari katika siku ya kuangamia kwako.