1. Neno la BWANA likanijia tena, kusema,
2. Na wewe, mwanadamu, mfanyie Tiro maombolezo;
3. umwambie Tiro, Ewe ukaaye penye maingilio ya bahari, uliye mchuuzi wa watu wa kabila nyingi, mpaka visiwa vingi, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe, Tiro, umesema, Mimi ni ukamilifu wa uzuri.
4. Mipaka yako i kati ya moyo wa bahari; wajenzi wako wameukamilisha uzuri wako.
5. Mbao zako zote wamezifanya kwa misunobari itokayo Seniri; wametwaa mierezi ya Lebanoni ili kukufanyia mlingoti;
6. kwa mialoni ya Bashani wamefanya makasia yako; na sitaha zako wamezifanya kwa pembe iliyotiwa kazi ya njumu katika mti wa mihugu itokayo Kitimu.
7. Tanga lako lilikuwa la kitani safi itokayo Misri, iliyotiwa taraza, ili iwe bendera kwako; na chandalua chako kilikuwa cha rangi ya samawi na urujuani toka visiwa vya Elisha.
8. Wakaao Sidoni na Arvadi ndio waliovuta makasia yako; wana wako wenye akili, Ee Tiro, walikuwa ndani yako, ndio waliokuwa rubani zako.
9. Wazee wa Gebali na wenye akili wake walikuwa ndani yako, wenye kutia kalafati; merikebu zote za bahari na mabaharia wao walikuwa ndani yako, ili kubadiliana biashara yako.
10. Watu wa Uajemi na Ludi na Putu walikuwa katika jeshi lako, watu wako wa vita; walitungika ngao na chapeo ndani yako; wakadhihirisha uzuri wako.
11. Watu wa Arvadi, pamoja na jeshi lako, walikuwa juu ya kuta zako pande zote, na Wagamadi walikuwa ndani ya minara yako; walitungika ngao zao juu ya kuta zako pande zote; wakaukamilisha uzuri wako.
12. Tarshishi alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa utajiri wa kila aina; kwa fedha, na chuma, na bati, na risasi, walifanya biashara, wapate vitu vyako vilivyouzwa.