11. Kwa kwato za farasi zake atazikanyaga njia zako zote; atawaua watu wako kwa upanga, na minara ya nguvu zako itashuka hata nchi.
12. Nao wataufanya utajiri wako kuwa mateka, na bidhaa yako kuwa mawindo; nao watazibomoa kuta zako, na kuziharibu nyumba zako zipendezazo; nao wataweka mawe yako, na miti yako, na mavumbi yako, kati ya maji.
13. Nami nitaikomesha sauti ya nyimbo zako, wala sauti ya vinubi vyako haitasikiwa tena.
14. Nami nitakufanya kuwa jabali tupu; utakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi; hutajengwa tena; maana mimi, BWANA, nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.
15. Bwana MUNGU amwambia Tiro neno hili; Je! Visiwa havitatikisika kwa mshindo wa kuanguka kwako, watakapougua waliojeruhiwa, yatakapofanyika machinjo kati yako.
16. Ndipo wakuu wote wa bahari watashuka kutoka viti vyao vya enzi, na kuweka upande mavazi yao, na kuvua nguo zao zilizotiwa taraza; watajivika matetemeko; wataketi na kutetemeka kila dakika, na kukustaajabia,
17. Nao watakufanyia maombolezo, na kukuambia, Imekuwaje wewe kuharibika, wewe uliyekaliwa na wana-maji, mji wenye sifa, uliyekuwa na nguvu katika bahari, mji huo, na hao waliokaa ndani yake, waliowatia hofu wote waliokaa ndani yake!