1. Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema,
2. Mwanadamu, Kwa sababu Tiro amesema juu ya Yerusalemu, Aha! Yeye amevunjika aliyekuwa lango la kabila za watu; amenigeukia; nitajazwa kwa kuwa sasa ameharibika;
3. basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi kupigana nawe, kama bahari iinuavyo mawimbi yake.
4. Nao wataziharibu kuta za Tiro, na kuibomoa minara yake; tena nitakwangua hata mavumbi yake yamtoke, na kumfanya kuwa jabali tupu.
5. Naye atakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi kati ya bahari; maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU; naye atakuwa mateka ya mataifa.
6. Na binti zake walio katika mashamba watauawa kwa upanga; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
7. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitamleta Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mfalme wa wafalme, juu ya Tiro toka kaskazini, pamoja na farasi, na magari ya vita, na wapanda farasi, na jeshi, na watu wengi.