11. Na umbu lake, Oholiba, akayaona hayo walakini alizidi kuharibika kuliko yeye, kwa kupendelea kwake, na kwa uzinzi wake, uliokuwa mwingi kuliko uzinzi wa umbu lake.
12. Aliwapendelea Waashuri, maliwali na mawaziri, jirani zake, waliovikwa nguo za shani, wapanda farasi wakipanda farasi zao, wote pia vijana wa kutamanika.
13. Nikaona ya kuwa ametiwa unajisi; wote wawili walifuata njia moja.
14. Naye akaongeza uzinzi wake; kwa maana aliona watu waume, ambao sura zao zimeandikwa ukutani, sura za Wakaldayo zilizoandikwa kwa rangi nyekundu;
15. waliofungiwa mikumbuu viunoni mwao, na vilemba vilivyotiwa rangi vichwani mwao; wote wakuu wa kuangaliwa, kwa mfano wa wana wa Babeli katika Ukaldayo, katika nchi ya kuzaliwa kwao.
16. Na mara alipowaona aliwapendelea, akatuma wajumbe kwao hata Ukaldayo.
17. Na watu wa Babeli wakamwendea katika kitanda cha mapenzi, wakamtia unajisi kwa uzinzi wao, akatiwa unajisi nao, kisha roho yake ikafarakana nao.
18. Basi alifunua uzinzi wake, na kufunua uchi wake; ndipo roho yangu ikafarakana naye, kama ilivyofarakana na umbu lake.
19. Lakini aliongeza uzinzi wake, akikumbuka siku za ujana wake, alipofanya mambo ya kikahaba katika nchi ya Misri.
20. Akawapendelea wapenzi wao, ambao nyama ya mwili wao ni kama nyama ya mwili wa punda, nacho kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi.
21. Ndivyo ulivyokumbuka uasherati wa ujana wako, yalipobanwa matiti yako na Wamisri, kwa maziwa ya ujana wako.
22. Kwa sababu hiyo, Ewe Oholiba, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, nitawainua wapenzi wako juu yako, ambao roho yako imefarakana nao, nami nitawaleta juu yako pande zote;
23. watu wa Babeli, na Wakaldayo wote, Pekodi na Shoa na Koa, na Waashuri wote pamoja nao; vijana wa kutamanika, wote pia, maliwali na mawaziri, wakuu, na watu wenye sifa, wote wenye kupanda farasi.
24. Nao watakuja kwako na silaha zao, na magari ya vita, na magurudumu, na wingi wa mataifa; watajipanga juu yako kwa ngao, na vigao, na chapeo za shaba, pande zote; nami nitawapa uwezo wa kuhukumu, nao watakuhukumu sawasawa na hukumu zao.