Eze. 22:1-11 Swahili Union Version (SUV)

1. Neno la BWANA likanijia tena, kusema,

2. Na wewe, mwanadamu, je! Utauhukumu, utauhukumu mji huu wa damu? Basi uujulishe machukizo yake yote.

3. Nawe utasema, Bwana MUNGU asema hivi; Mji umwagao damu ndani yake, ili wakati wake upate kuja; mji ufanyao vinyago juu ya nafsi yake, ili ujitie unajisi!

4. Umekuwa na hatia katika damu yako uliyomwaga, nawe umekuwa na unajisi kwa vinyago vyako ulivyovifanya; nawe umezileta karibu siku zako, nawe umefika karibu na miaka yako; basi, kwa sababu ya hayo, nimekufanya kuwa lawama kwa mataifa, na kuwa dhihaka katika nchi zote.

5. Zilizo karibu, na zilizo mbali nawe, zitakudhihaki, Ewe mchafu, uliyejaa fujo.

6. Tazama, wakuu wa Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya nguvu zake, wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu.

7. Ndani yako wamedharau baba na mama; kati yako wamewatenda wageni udhalimu; ndani yako wamewaonea yatima na mjane.

8. Umevidharau vitu vyangu vitakatifu, umezitia unajisi sabato zangu.

9. Wasingiziaji wamekuwamo ndani yako, ili kumwaga damu; na ndani yako wamekula juu ya milima; kati yako wamefanya uasherati.

10. Ndani yako wamefunua uchi wa baba zao; ndani yako wamemfanyia nguvu mwanamke asiye safi wakati wa kutengwa kwake.

11. Na mtu mmoja amefanya chukizo pamoja na mke wa jirani yake; na mtu mwingine amemharibu mke wa mwanawe kwa uasherati; na mtu mwingine ndani yako amemfanyia nguvu umbu lake, binti ya babaye.

Eze. 22