4. Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hata kaskazini,
5. na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena.
6. Ugua, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika kwake viuno vyako, na kwa uchungu, utaugua mbele ya macho yao.
7. Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unaugua? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatalegea kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU.
8. Neno la BWANA likanijia, kusema,
9. Mwanadamu, tabiri, useme, BWANA asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa,
10. umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti.
11. Nao umenolewa usuguliwe, upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye.