11. Nao umenolewa usuguliwe, upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye.
12. Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani.
13. Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU.
14. Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote.
15. Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje.
16. Jiweke tayari, enenda upande wa kuume; jipange, enenda upande wa kushoto; mahali po pote utakapouelekeza uso wako.
17. Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, BWANA, nimenena neno hili.