Eze. 19:1-9 Swahili Union Version (SUV)

1. Tena uwaombolezee wakuu wa Israeli,

2. useme, Mama yako alikuwa nini? Simba mke; alijilaza kati ya simba, kati ya wana-simba aliwalisha watoto wake.

3. Akamlea mtoto mmoja katika watoto wake, akawa mwana-simba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu.

4. Mataifa nao wakapata habari zake, akanaswa katika rima lao, wakamchukua kwa kulabu mpaka nchi ya Misri.

5. Basi mamaye alipoona kwamba amemngoja, na tumaini lake limepotea, akatwaa mtoto mwingine katika watoto wake, akamfanya mwana-simba.

6. Naye akaenda huko na huko kati ya simba, akawa mwana-simba, akajifunza kuwinda mawindo, akala watu.

7. Akayajua majumba yao, akaiharibu miji yao; nchi ikawa ukiwa, navyo vitu vilivyoijaza, kwa sababu ya mshindo wa kunguruma kwake.

8. Ndipo mataifa wakajipanga juu yake pande zote toka nchi zote; wakaunda wavu wao juu yake; akanaswa katika rima lao.

9. Wakamtia katika tundu kwa kulabu, wakamleta kwa mfalme wa Babeli wakamtia ndani ya ngome, sauti yake isisikiwe tena juu ya milima ya Israeli.

Eze. 19