1. Neno la BWANA likanijia, kusema,
2. Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli mithali;
3. useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tai mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya marefu katika mabawa, mwenye kujaa manyoya, yaliyo ya rangi mbalimbali, alifika Lebanoni, akakitwaa kilele cha mwerezi;
4. akakikata kitawi kilicho juu katika vitawi vyake, akakichukua mpaka nchi ya biashara, akakiweka katika mji wa wachuuzi.
5. Akatwaa tena mbegu katika mbegu za nchi hiyo, akaipanda katika udongo uzaao sana, akaiweka kando ya maji mengi; aliipandikiza kama mti ukuao karibu na mto.
6. Ikakua, ikawa mzabibu wenye kuenea sana, wa kimo kifupi, ambao matawi yake yalimgeukia, na mizizi yake ilikuwa chini yake; basi ukawa mzabibu, ukatoa matawi, ukachipuza vichipuko.
7. Kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya mengi; na tazama, mzabibu huo ukapinda mizizi yake imwelekee yeye, ukachipuza matawi yake yamwelekee yeye, toka matuta yake ulipopandwa; ili yeye apate kuunywesha.
8. Ulikuwa umepandwa katika udongo mwema, kando ya maji mengi, upate kutoa matawi, na kuzaa matunda, uwe mzabibu mzuri.
9. Basi nena wewe, Bwana MUNGU asema hivi; Je! Huo utafanikiwa? Yeye hataing’oa mizizi yake na kuyakata matunda yake, ili ukauke? Kwamba majani mabichi yake yote yachipukayo yakauke, hata ikiwa hana nguvu nyingi, wala watu wengi wa kuung’oa na mizizi yake?
10. Naam, tazama, ingawa umepandwa, je! Utafanikiwa? Hautakauka kabisa, upepo wa mashariki utakapoupiga? Naam, utakauka katika matuta hapo ulipopandwa.
11. Tena neno la BWANA likanijia, kusema,
12. Waambie sasa nyumba hii iliyoasi, Hamjui maana ya mambo haya? Waambie, Tazama, mfalme wa Babeli alifika Yerusalemu, akamtwaa mfalme wake, na wakuu wake, akawachukua pamoja naye mpaka Babeli;
13. akawatwaa baadhi ya wazao wa kifalme; kisha akafanya agano naye, akamwapisha; akawaondoa watu wa nchi wenye nguvu;