50. Nao walijivuna, wakafanya machukizo mbele zangu; kwa sababu hiyo naliwaondoa hapo nilipoyaona.
51. Samaria naye hakutenda nusu ya dhambi zako; bali wewe umeyaongeza machukizo yako zaidi ya hao, nawe umewapa haki maumbu yako kwa machukizo yako yote uliyoyatenda.
52. Wewe nawe, ichukue aibu yako mwenyewe, kwa kuwa umetoa hukumu juu ya maumbu yako; kwa dhambi zako ulizozitenda, zilizochukiza kuliko hao, wao wana haki kuliko wewe; naam, ufedheheke wewe nawe, ukaichukue aibu yako, kwa kuwa umewapa haki maumbu yako.
53. Nami nitawarudisha watu wao waliofungwa; wafungwa wa Sodoma na binti zake, na wafungwa wa Samaria na binti zake na wafungwa wako waliofungwa kati yao;
54. upate kuichukua aibu yako mwenyewe, na kutahayari, kwa sababu ya mambo yote uliyoyatenda, kwa kuwa umekuwa faraja kwao.
55. Na maumbu yako, Sodoma na binti zake, watairudia hali yao ya kwanza, na Samaria na binti zake watairudia hali yao ya kwanza, na wewe na binti zako mtairudia hali yenu ya kwanza.
56. Kwa maana umbu lako, Sodoma, hakutajwa kwa kinywa chako katika siku ya kiburi chako;
57. kabla uovu wako haujafunuliwa bado, kama vile wakati ule walipokutukana binti za Shamu, na wale wote waliomzunguka, binti za Wafilisti wanaokudharau pande zote.
58. Umeuchukua uasherati wako, na machukizo yako, asema BWANA.
59. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitakutenda vile vile kama ulivyotenda, uliyekidharau kiapo kwa kulivunja agano.
60. Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe.
61. Hapo ndipo utakapozikumbuka njia zako, na kutahayarika, hapo utakapowakaribisha maumbu yako, walio wakubwa wako na wadogo wako; nami nitakupa hao wawe binti zako, lakini si kwa agano lako.
62. Nami nitaweka imara agano langu nawe; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi BWANA;
63. upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aibu yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana MUNGU.