48. Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, Sodoma, umbu lako, yeye na binti zake, hawakutenda kama wewe ulivyotenda, wewe na binti zako.
49. Tazama, uovu wa umbu lako, Sodoma, ulikuwa huu; kiburi, na kushiba chakula, na kufanikiwa, hayo yalikuwa ndani yake na binti zake; tena hakuutia nguvu mkono wa maskini na mhitaji.
50. Nao walijivuna, wakafanya machukizo mbele zangu; kwa sababu hiyo naliwaondoa hapo nilipoyaona.
51. Samaria naye hakutenda nusu ya dhambi zako; bali wewe umeyaongeza machukizo yako zaidi ya hao, nawe umewapa haki maumbu yako kwa machukizo yako yote uliyoyatenda.
52. Wewe nawe, ichukue aibu yako mwenyewe, kwa kuwa umetoa hukumu juu ya maumbu yako; kwa dhambi zako ulizozitenda, zilizochukiza kuliko hao, wao wana haki kuliko wewe; naam, ufedheheke wewe nawe, ukaichukue aibu yako, kwa kuwa umewapa haki maumbu yako.
53. Nami nitawarudisha watu wao waliofungwa; wafungwa wa Sodoma na binti zake, na wafungwa wa Samaria na binti zake na wafungwa wako waliofungwa kati yao;
54. upate kuichukua aibu yako mwenyewe, na kutahayari, kwa sababu ya mambo yote uliyoyatenda, kwa kuwa umekuwa faraja kwao.