Eze. 16:27-37 Swahili Union Version (SUV)

27. Basi, tazama, kwa ajili ya hayo nimenyosha mkono wangu juu yako, nami nimelipunguza posho lako, na kukutoa kwa mapenzi yao wanaokuchukia, binti za Wafilisti, walioyaonea haya mambo yako ya uasherati.

28. Pia umefanya mambo ya kikahaba pamoja na Waashuri, kwa sababu ulikuwa huwezi kushibishwa; naam, umefanya mambo ya kikahaba pamoja nao, wala hujashiba bado.

29. Pamoja na hayo umeongeza mambo yako ya kikahaba katika nchi ya Kanaani, mpaka Ukaldayo, wala hujashibishwa kwa hayo.

30. Jinsi moyo wako ulivyokuwa dhaifu, asema Bwana MUNGU, ikiwa unafanya mambo hayo yote, kazi ya mwanamke mzinzi,

31. apendaye kutawala watu; kwa kuwa wajijengea mahali pako pakuu penye kichwa cha kila njia, na kufanya mahali pako palipoinuka katika kila njia kuu; lakini hukuwa kama kahaba, kwa maana ulidharau kupokea ujira.

32. Mke wa mtu, aziniye! Akaribishaye wageni badala ya mumewe!

33. Watu huwapa makahaba wote zawadi, bali wewe unawapa wapenzi wako wote zawadi zako, na kuwapa rushwa ili waje kwako pande zote, kwa ajili ya mambo yako ya kikahaba.

34. Tena, katika mambo yako ya kikahaba, wewe na wanawake wengine ni mbalimbali, kwa kuwa hapana akufuataye katika mambo yako ya kikahaba; tena kwa kuwa unatoa ujira, wala hupewi ujira; basi, njia yako na njia yao ni mbalimbali.

35. Kwa sababu hiyo, Ewe kahaba, lisikie neno la BWANA;

36. Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu uchafu wako umemwagwa, na uchi wako umefunuliwa, kwa njia ya uzinzi wako pamoja na wapenzi wako; na kwa sababu ya vinyago vyote vya machukizo yako; na kwa sababu ya damu ya watoto wako, uliyowapa;

37. basi, tazama, nitawakusanya wapenzi wako wote ambao umejifurahisha pamoja nao, nao wote uliowapenda, pamoja na watu wote uliowachukia; naam, nitawakusanya juu yako pande zote, na kuwafunulia uchi wako, wapate kuuona uchi wako wote.

Eze. 16