11. basi waambie hao wanaoupaka ukuta chokaa isiyokorogwa vema, ya kwamba utaanguka; kutakuwa mvua ya kufurika; nanyi, enyi mvua ya mawe makubwa ya barafu, mtaanguka; na upepo wa dhoruba utaupasua.
12. Na huo ukuta utakapoanguka, je! Hamtaambiwa, Ku wapi kupaka kwenu mlikoupaka?
13. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Nitaupasua kwa upepo wa dhoruba, katika ghadhabu yangu; tena kutakuwa mvua ya barafu ya kufurika katika hasira yangu; na mawe makubwa ya barafu katika hasira ya kuukomesha.
14. Ndivyo nitakavyoubomoa ukuta mlioupaka chokaa isiyokorogwa vema, na kuuangusha chini, hata misingi yake itafunuliwa; nao utaanguka, nanyi mtaangamizwa katikati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
15. Ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu juu ya ukuta ule, na juu yao walioupaka chokaa isiyokorogwa vema; nami nitawaambieni, Ukuta huo hauko sasa, wala wao walioupaka hawako;
16. yaani, manabii wa Israeli, watabirio habari za Yerusalemu, na kuona maono ya amani katika habari zake; wala hapana amani, asema Bwana MUNGU.
17. Na wewe, mwanadamu, kaza uso wako juu ya binti za watu wako, watabirio kwa akili zao wenyewe; ukatabiri juu yao,
18. useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe?