15. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; nitakapowatawanya kati ya mataifa, na kuwatupa-tupa katika nchi zote.
16. Lakini nitawasaza watu wachache miongoni mwao na kuwaokoa na upanga, na njaa, na tauni ili watangaze habari ya machukizo yao yote, kati ya mataifa huko waendako; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
17. Tena neno la BWANA likanijia, kusema,
18. Mwanadamu, ule chakula chako kwa matetemo, ukanywe maji yako kwa kutetemeka na kwa kuyatunza sana;
19. ukawaambie watu wa nchi, Bwana MUNGU asema hivi, katika habari zao wakaao Yerusalemu, na katika nchi ya Israeli; Watakula chakula chao kwa kukitunza sana, na maji yao watayanywa kwa ushangao, nchi yao iwe ukiwa, kwa kukosa vitu vyote viijazavyo, kwa sababu ya udhalimu wao wote wakaao ndani yake.
20. Na miji yote yenye watu itakuwa maganjo, nayo nchi itakuwa ukiwa; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
21. Neno la BWANA likanijia, kusema,
22. Mwanadamu, ni mithali gani hii mliyo nayo katika nchi ya Israeli, mkisema, Siku hizo zinakawia na maono yote hayatimizwi.
23. Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Nitaikomesha mithali hii, wasiitumie tena kama mithali katika Israeli; lakini uwaambie, Siku hizo ni karibu, na utimilizo wa maono yote.
24. Kwa maana hayatakuwapo tena maono yo yote ya ubatili, wala ubashiri wa kujipendekeza, katika nyumba ya Israeli.