8. Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi;
9. mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele.
10. Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng’ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia.
11. Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao.
12. Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda.
13. Kwa habari za kuonekana kwao vile viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya vile viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme.
14. Na vile viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme.