17. Yalipokwenda yalikwenda pande zote nne; hayakugeuka yalipokwenda.
18. Katika habari za vivimbe vyake; vilikuwa virefu, vya kutisha; nayo yote manne, vivimbe vyake vimejaa macho pande zote.
19. Na viumbe hao walipokwenda, magurudumu yalikwenda kandokando yao, na viumbe hao walipoinuliwa, magurudumu nayo yaliinuliwa.
20. Kila mahali ambako roho hiyo ilitaka kwenda, walikwenda; walikuwa na roho ya kwenda huko; nayo magurudumu yaliinuliwa karibu nao; kwa maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu.
21. Walipokwenda hao, yalikwenda hayo nayo; na waliposimama hao, yalisimama hayo nayo; na walipoinuliwa hao juu ya nchi, magurudumu yaliinuliwa karibu nao; maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu.
22. Tena juu ya vichwa vya viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa anga, kama rangi ya bilauri, lenye kutisha, limetandwa juu ya vichwa vyao.
23. Na chini ya anga mabawa yao yamenyoshwa, moja kulielekea la pili; kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande mmoja, na kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande wa pili.