Eze. 1:10-26 Swahili Union Version (SUV)

10. Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng’ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia.

11. Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao.

12. Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda.

13. Kwa habari za kuonekana kwao vile viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya vile viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme.

14. Na vile viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme.

15. Basi, nilipokuwa nikivitazama vile viumbe hai, tazama, gurudumu moja juu ya nchi, karibu na kila kimoja cha vile viumbe hai, pande zake zote nne.

16. Kuonekana kwake magurudumu hayo na kazi yake kulikuwa kama rangi ya zabarajadi; nayo yote manne yalikuwa na mfano mmoja; na kuonekana kwake na kazi yake kulikuwa kana kwamba ni gurudumu ndani ya gurudumu lingine.

17. Yalipokwenda yalikwenda pande zote nne; hayakugeuka yalipokwenda.

18. Katika habari za vivimbe vyake; vilikuwa virefu, vya kutisha; nayo yote manne, vivimbe vyake vimejaa macho pande zote.

19. Na viumbe hao walipokwenda, magurudumu yalikwenda kandokando yao, na viumbe hao walipoinuliwa, magurudumu nayo yaliinuliwa.

20. Kila mahali ambako roho hiyo ilitaka kwenda, walikwenda; walikuwa na roho ya kwenda huko; nayo magurudumu yaliinuliwa karibu nao; kwa maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu.

21. Walipokwenda hao, yalikwenda hayo nayo; na waliposimama hao, yalisimama hayo nayo; na walipoinuliwa hao juu ya nchi, magurudumu yaliinuliwa karibu nao; maana roho ya viumbe hai ilikuwa ndani ya magurudumu.

22. Tena juu ya vichwa vya viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa anga, kama rangi ya bilauri, lenye kutisha, limetandwa juu ya vichwa vyao.

23. Na chini ya anga mabawa yao yamenyoshwa, moja kulielekea la pili; kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande mmoja, na kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande wa pili.

24. Nao walipokwenda nalisikia mshindo wa mabawa yao, kama mshindo wa maji makuu, kama sauti yake Mwenyezi, mshindo wa mvumo, kama mshindo wa jeshi; hapo waliposimama walishusha mabawa yao.

25. Tena palikuwa na sauti juu ya anga lile, lililokuwa juu ya vichwa vyao; hapo waliposimama walishusha mabawa yao.

26. Na juu ya anga, lililokuwa juu ya vichwa vyao, palikuwa na mfano wa kiti cha enzi, kuonekana kwake kama yakuti samawi; na juu ya mfano huo wa kiti cha enzi, ulikuwako mfano kama kuonekana kwa mfano wa mwanadamu juu yake.

Eze. 1