2. Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo.
3. Mfalme akamwambia, Malkia Esta, wataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme.
4. Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia.
5. Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyosema. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta.
6. Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa.
7. Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii,
8. Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunifanyizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema.
9. Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kutetemeka mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai.
10. Walakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi mkewe.