1. Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye.
2. Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala kumsujudia.
3. Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme?
4. Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi.
5. Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana.
6. Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai.
7. Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari.