1. Baada ya hayo, hasira yake mfalme Ahasuero ilipotulia, alimkumbuka Vashti, na vile alivyotenda, na yale yaliyoamriwa juu yake.
2. Basi watumishi wa mfalme waliomhudumu walimwambia, Mfalme na atafutiwe mabikira vijana wazuri;
3. naye mfalme aweke wasimamizi katika majimbo yote ya ufalme wake, ili wakusanye pamoja mabikira vijana wazuri wote waende Shushani ngomeni, kwenye nyumba ya wanawake mikononi mwa Hegai, msimamizi-wa-nyumba wa mfalme, mwenye kuwalinda wanawake; tena wapewe vifaa vya utakaso.
4. Naye yule msichana atakayempendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti. Neno hilo likampendeza mfalme, naye akafanya hivyo.