Est. 1:7-13 Swahili Union Version (SUV)

7. Wakawanywesha kileo katika vyombo vya dhahabu, na vile vyombo vilikuwa mbalimbali, na divai tele ya namna ya kifalme, sawasawa na ukarimu wa mfalme;

8. kunywa kulikuwa kama ilivyoamriwa, bila sharti; maana ndivyo mfalme alivyowaagiza watumishi-wa-nyumbani, kila mtu afanye apendavyo.

9. Tena Vashti, malkia, naye akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero.

10. Hata siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero,

11. wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso.

12. Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake.

13. Basi mfalme akawaambia wenye hekima, walio na elimu ya nyakati; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu;

Est. 1