11. wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso.
12. Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake.
13. Basi mfalme akawaambia wenye hekima, walio na elimu ya nyakati; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu;
14. na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale maakida saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza,
15. Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba?
16. Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero.
17. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja.