Efe. 6:6-18 Swahili Union Version (SUV)

6. wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo;

7. kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu;

8. mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru.

9. Nanyi, akina bwana, watendeeni wao yayo hayo, mkiacha kuwaogofya, huku mkijua ya kuwa yeye aliye Bwana wao na wenu yuko mbinguni, wala kwake hakuna upendeleo.

10. Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

11. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15. na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16. zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;

18. kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

Efe. 6