Ebr. 11:26-36 Swahili Union Version (SUV)

26. akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.

27. Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.

28. Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao.

29. Kwa imani wakapita kati ya Bahari ya Shamu, kama katika nchi kavu; Wamisri walipojaribu kufanya vivyo wakatoswa.

30. Kwa imani kuta za Yeriko zikaanguka, zilipokwisha kuzungukwa siku saba.

31. Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani.

32. Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii;

33. ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba,

34. walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.

35. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora;

36. wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;

Ebr. 11