Ebr. 11:16-29 Swahili Union Version (SUV)

16. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji.

17. Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee;

18. naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa,

19. akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.

20. Kwa imani Isaka akawabariki Yakobo na Esau, hata katika habari ya mambo yatakayokuwa baadaye.

21. Kwa imani Yakobo, alipokuwa katika kufa, akambariki kila mmoja wa wana wa Yusufu, akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.

22. Kwa imani Yusufu, alipokuwa amekaribia mwisho wake, alitaja habari za kutoka kwao wana wa Israeli, akaagiza kwa habari ya mifupa yake.

23. Kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona kwamba ni mtoto mzuri; wala hawakuiogopa amri ya mfalme.

24. Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;

25. akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;

26. akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.

27. Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.

28. Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao.

29. Kwa imani wakapita kati ya Bahari ya Shamu, kama katika nchi kavu; Wamisri walipojaribu kufanya vivyo wakatoswa.

Ebr. 11