10. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
11. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi.
12. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu;
13. tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake.
14. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa.
15. Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema,
16. Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana,Nitatia sheria zangu mioyoni mwao,Na katika nia zao nitaziandika;ndipo anenapo,
17. Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa.
18. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.
19. Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu,
20. njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake;
21. na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu;
22. na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi.
23. Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu;
24. tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri;
25. wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.
26. Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi;