2. Nami naliona katika maono; ilitukia, nilipoona, nalikuwako huko Shushani ngomeni, katika wilaya ya Elamu; nikaona katika maono, nami nalikuwa karibu na mto Ulai.
3. Ndipo nikainua macho yangu nikaona, na tazama, mbele ya mto alisimama kondoo mume, mwenye pembe mbili; na pembe zile mbili zilikuwa ndefu; lakini moja ilikuwa ndefu kuliko ya pili, na ile iliyokuwa ndefu zaidi ilizuka mwisho.
4. Nikamwona huyo kondoo mume akisukuma upande wa magharibi, na upande wa kaskazini, na upande wa kusini; wala hakuna mnyama ye yote awezaye kusimama mbele yake, wala hakuna mnyama ye yote awezaye kupokonya mkononi mwake; lakini alitenda kama alivyopenda mwenyewe, akajitukuza nafsi yake.
5. Nami nilipokuwa nikifikiri, tazama, beberu akatoka upande wa magharibi, juu ya uso wa dunia nzima, bila kuigusa nchi; na beberu yule alikuwa na pembe mashuhuri kati ya macho yake.
6. Naye akamwendea huyo kondoo mume mwenye pembe mbili, niliyemwona akisimama karibu na mto, akamshambulia kwa ghadhabu za nguvu zake.
7. Nikamwona akimkaribia kondoo mume, akamwonea hasira kali, akampiga kondoo mume, akazivunja pembe zake mbili; na huyo kondoo mume alikuwa hana nguvu kusimama mbele yake; bali akamwangusha chini, akamkanyaga-kanyaga; wala hapakuwapo awezaye kumwokoa kondoo mume katika mkono wake.